NA JOYCE KASIKI,DODOMA
Wizara ya Afya kwa kushirikiana Ofisi
ya Rais TAMISEMI na Wadau wa Sekta ya Afya inatarajia kuendesha Kampeni ya
kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio kwa watoto zaidi ya Milioni 3.2 walio
chini ya miaka 8 ili kuwakinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari
kuhusu kampeni hiyo inayotarajiwa kuanza kutolewa kwenye Mikoa sita ya Rukwa,
Kagera, Kigoma, Katavi, Songwe na Mbeya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema,kampeni
hiyo ni kufuatia kuwepo kwa mtoto mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi
kumi na moja Sumbawanga katika mkoa wa Rukwa ambaye alipooza ghafla na tayari amethibitika
kimaabara kwamba ana virus vya polio.
“Kampeni hii tunaanza na mikoa hiyo
sita kwanza kwa sababu imezungukwa na nchi za Burundi ,Zambia na Demokrasia ya
Congo,na kufuatia hali hii Tanzania inakuwa katika hatari ya kupata
maambukizi ya polio hasa katika mikoa
iliyozungukwa na nchi hizo.”amesema Ummy na
Kwa mujibu wa Ummy taarifa za
kitakwimu zinaonyesha kuwa akiwepo mtoto mmoja mwenye ugonjwa wa polio ,nyuma
yake kunakuwa na watoto 200 wenye polio ambapo mmoja anaweza kupata ulemavu wa
kudumu na kwamba katika kila watoto kumi mtoto mmoja ataonyesha dalili za
ugonjwa huo.
“Kwa hiyo napenda nichukue fursa hii
kuwataarifu kuwa tutakuwa na Kampeni maalum ya utoaji wa chanjo ya matone dhidi
ya Polio (nOPV2) kwa watoto wote wenye umri chini ya miaka minane ambayo
itafanyika kwa siku nne kuanzia Septemba 21 – 24 Septemba, 2023 katika mikoa
hiyo sita kampeni ambayo itafanyika nyumba kwa nyuma,katika mikusanyiko na
nyumba za Ibadan a shuleni,
“Lengo la kampeni hii ni kuwafikia watoto
3,250,598 waliozaliwa baada ya mwaka 2016 ili kuwakinga dhidi ya Kirusi cha
Polio aina ya pili kinachoweza kusababisha
ulemavu wa kudumu ambapo kwa mkoa Rukwa tunatarajia kuwafikia watoto 391,883
Kagera 729,387 Kigoma 884,477 Mbeya 614,346 Katavi 227,862 na Songwe
402,643”. amefafanua Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema Ili kufanikisha
Kampeni hii, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI pamoja na Wadau wa
chanjo imeshafanya maandalizi kwa ajili ya kuwezesha zoezi bila kuathiri
shughuli zingine za wananchi.
“Wakati wa Kampeni kutakuwa na jumla
ya timu yenye jumla ya watoa huduma za afya 5,291 kwa Mikoa yote sita
itakayofikiwa na zoezi hili ambapo kila timu itakuwa na watoa huduma watatu.
Timu hizi zitakuwa zinatoa huduma ya chanjo kwa walengwa kupitia vituo vya kutolea
huduma za afya, nyumba kwa nyumba, shuleni na maeneo mbalimbali ya mikusanyiko
ikiwemo Nyumba za Ibada”.
Ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa
wazazi na walezi kutoa ushirikiano kwa watoa huduma za afya ili kuwezesha
watoto wao kuchanjwa kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba huku akiuhakikishia
umma kuwa chanjo hiyo ni salama.
Vile vile amewataka waganga wakuu wa
Mikoa kuhakikisha chanjo zipo za kutosha ili watoto wote waliolengwa waweze
kufikiwa lakini pia amewataka waimarishe maelekezo ya utoaji elimu kwa umma ili
jamii ielewe kuhusu kampeni ya chanjo hiyo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa
Serikali Prof. Tumaini Nagu amesema katika kuendeleza mikakati ya kutoa chanjo
dhidi ya Polio, imeundwa timu ya watu waliopata mafunzo ya kutoa chanjo hiyo
katika Mikoa hiyo sita.
“Tumeunda timu nzuri ambayo imepata
mafunzo ya kutoa chanjo ambayo ina watoa huduma Elfu Tano Mia Mbili Tisini
na Moja katika Mikoa hiyo Sita ili
kuhakikisha watoto wote wanafikiwa katika kupatiwa Chanjo dhidi ya ugonjwa wa
Polio” amesema Prof. Nagu amesema na kuongeza kuwa
“Tunawapa hamasa wazazi wahakikishe
kwamba, wanawatoa watoto wao kupata chanjo hii ili kuwaepusha watoto wetu
kupata ulemavu ambao kwakweli unakingika kwa kutumia chanjo”. Ameongezea Prof.
Nagu.
Tanzania inaendesha Kampeni hiyo ya
chanjo kutokana na Wizara kupokea taarifa mnamo Mei 26, 2023 za uwepo wa mtoto
mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kumi na moja ambaye alionyesha dalili
za kupooza kwa ghafla.
Mtoto huyo ambaye alitolewa taarifa
kutoka Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa. Uchunguzi wa Maabara umethibitisha
kuwa mtoto huyo ana maambukizi ya virusi cha Polio.
No comments:
Post a Comment